Wednesday, September 17, 2014

STEWART HALL AIPONDA AZAM FC, DOMAYO AKIRI YANGA NI NOOOMA

Wakati aliyekuwa kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall akishangazwa na kiwango kidogo cha timu hiyo katika mchezo wao wa juzi wa Ngao ya Hisani, kiungo wa Taifa Stars, Frank Domayo amekiri kuzidiwa uwezo na Yanga.

Hall, aliyekuwa miongoni mwa maelfu ya mashabiki walioushuhudia Azam ikilala kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, alisema timu hiyo ilicheza chini ya kiwango katika mchezo huo hasa kipindi cha pili ambacho waliruhusu mabao yote matatu.


“Azam iliyocheza leo (juzi) si ile ambayo naifahamu. Imecheza vibaya na chini ya kiwango, kama uchezaji wao ndio huu, inapaswa kufanya kazi ya ziada kwenye ligi,” alisema Hall kwa kifupi na kuondoka uwanjani hapo.

Naye Domayo, ambaye amehamia Azam akitokea Yanga, alisema timu yake ya zamani iliwazidi mbinu hasa kipindi cha pili na kujikuta wakikubali kipigo hicho.

“Tulizidiwa mbinu hasa kipindi cha pili, wenzetu walirudi vizuri na kucheza kwa kushambulia zaidi tofauti na sisi ambao baadhi ya wachezaji walichoka kipindi cha pili,” alisema Domayo ambaye hakucheza mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.