Wednesday, September 17, 2014

DIAMOND,FLAVOUR KUSHIRIKI TENA KUINADI COKE STUDIO

Mwanamuziki nyota nchini, Diamond Platnumz na Flavour kutoka Nigeria watashiriki katika msimu wa pili wa promosheni ya Coke Studio.

Kipindi cha Coke Studio kinaonyesha namna wanamuziki wanavyoweza kuimba jukwaani na muziki ukipigwa moja kwa moja.

Katika promosheni hiyo wanamuziki hao wa Tanzania watashirikiana na wenzao kutoka Kenya, Uganda, Nigeria na Msumbiji na kuonyesha moja kwa moja kwenye televisheni za nchini hizo kila Jumamosi.

Diamond, Joe Makini, Shaa na Vanessa Mdee wataiwakilisha Tanzania na kutoka Nigeria watakuwapo Flavour Nabania, Omawumi, Waje, Burna Boy, Chidima, Olamide, Iyanya, Seyi Shay, Yemi Alade na Phyno.


Wengine ni Fena Gitu, Rabbit, Victoria Kimani na Jay A kutoka Kenya; Navio, Jackie Chandiru na Lillian Mbabazi kutoka Uganda; Neyma, Jose Valdemiro na Marllen kutoka Msumbiji.

Watayarishaji wa muziki maarufu kama Silvastone kutoka Ghana, Chopstix na Afrologic kutoka Nigeria, Kevin Provoke, Kagwe Mugai na Owuor Arunga kutoka Kenya pia wamejumuishwa katika uandaaji wa kipindi cha Coke Studio.

Meneja Coca-Cola Tanzania, Maurice Njowoka alisema promosheni hiyo ni kwa ajili ya vinywaji vya Coca-Cola za chupa zenye ujazo wa 200ml, 300ml na 350ml.

Njowoka alisema Coca-Cola imeamua kushirikiana na Vodacom ili wateja wa Coca-Cola kujishindia muda wa maongezi wa dakika tano kwa chupa ya soda wanayonunua.