Monday, September 1, 2014

MOSOTI AKATAA KUONDOKA SIMBA

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Beki Mkenya Donald Mosoti amesema hataondoka Simba mpaka kieleweke kwa kuwa hajui lolote kuhusu kuondolewa katika timu hiyo.

Kumekuwapo na taarifa za kuondolewa kwa beki huyo baada ya Simba kumsajili mshambuliaji Emmanuel Okwi aliyekuwa akiichezea Yanga na hivyo idadi ya wachezaji wa kigeni kuzidi idadi ya wachezaji watano katika timu hiyo.

Klabu za Ligi Kuu zinatakiwa kuwa na wachezaji watano tu wa kigeni, lakini Simba hivi sasa ina wachezaji sita ambao ni Amissi Tambwe, Raphael Kiongera, Pierre Kwizera, Joseph Owino, Donald Mosoti na Emmanuel Okwi, kwa hiyo italazimika kumpunguza mmoja.


Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa tayari suala la kumpunguza Mosoti limepitishwa ili kumpa nafasi Okwi, ingawa usajili wake bado una utata baada ya Yanga kueleza kuwa haijavunja mkataba na Okwi.

Pia jina la mshambuliaji huyo wa Uganda limo katika orodha yao ya usajili waliyoipeleka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Akizungumza na gazeti hili, Mosoti alisema kuwa amekutana na viongozi wa Simba waliokuja kushuhudia mechi yao ya kirafiki dhidi ya KMKM iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Amaan, lakini hakuna hata mmoja aliyezungumzia taarifa za yeye kuachwa.

“Mimi ni mchezaji wa kigeni, hizo taarifa za kuachwa nimezisikia kupitia mitandao na vyombo vya habari, hata kwetu Kenya wamenipigia simu, lakini nashindwa kuwaambia kama ni kweli au uongo.

“Nasema hivyo kwa sababu kama ni kweli, viongozi wangu walitakiwa kunipa barua rasmi, lakini sijapewa na wala sijaambiwa lolote, hivyo bado najihesabia ni mchezaji wao. Ikitokea wamenipa barua nikasoma na kuielewa, ndipo nitakuwa na neno la kuzungumza zaidi,” alisema Mosoti.

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa aliondoleawa baada ya kuomba kuvunjwa kwa mkataba wake ili aende kucheza katika moja ya timu nchini Qatar.

Mjumbe wa Kamati ya Usajili, Said Tully alisema kuwa “kila jambo tunafanya kwa utaratibu. Bado kuna muda wa usajili kwa wachezaji wa kigeni, lakini timu yetu ndiyo hiyo iliyocheza juzi na KMKM ukimtoa Mosoti”.

Alisema: “Kuna taratibu zitafanywa halafu Mosoti ataambiwa kwani mambo mengine lazima yaamuliwe na rais wetu wa Simba, Evans Aveva ambaye kwa sasa amesafiri. Akirudi kila kitu kitakuwa sawa,” alisema.

Katika kikosi cha Simba, beki Joram Mgeveke ndiye anayecheza nafasi moja na Mosoti, lakini bado kocha Patrick Phiri hajamwamini sana kama ilivyo kwa Mosoti kwa madai kuwa bado hana uzoefu mkubwa katika ligi.