Monday, September 1, 2014

Wasanii watishia kutopiga kura katiba mpya

Msanii John Kitime (mwenye miwani) akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya ujumbe wa wasanii wenzake waliokutana na kamati za Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma kwa ajili ya kutaka masuala yahusuyo wasanii yaingizwe kwenye Katiba itakayopendekezwa na bunge hilo jana. Kulia ni Rais wa Shirikisho la Wasanii, Simon Mwakifamba . (PICHA: SELEMANI MPOCHI)
 
Viongozi wa wasanii nchini wamesema hawataipigia kura katiba mpya kama wajumbe wa Bunge maalum la katiba hawataingiza ndani vipengele vya kuwatambua.

Akizungumza mjini Dodoma jana, mwenyekiti wa ujumbe wa wasanii hao, John Kitime, alisema tayari wamekutana na wajumbe hao na kuwaelezea msimamo wao huo.

Alisema katika mchakato wa kutafuta katiba ya mpya kuna mambo ya msingi ambayo kama wasanii wanataka yaingizwe ili kuwalinda na kutambulika.

Alitaja vipengele wanavyotaka viongezwe ni katiba kutambua wasanii ni kundi maalum, pamoja na kuingizwa kifungu kinacholinda mali zisizoshikika.

“Tumekutana na kambi zote, tumewaambia tunataka mambo haya yawekwe kwenye katiba mpya, ikishindikana hatutapiga kura,” alisema Kitime.

Kwa upande wa Rais wa Shirikisho la Wasanii (TAFF), Simon Mwakifwamba, alitoa wito kwa wajumbe wa wanaounda umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa) kurejea bungeni.

Alisema katiba inayotafutwa ni kwa ajili ya wananchi wote, hivyo kunahitajika kuwapo na maridhiano yatakayoleta umoja na mshikamano katika nchi.

Chanzo      Nipashe