Friday, September 5, 2014

Remy apiga bao maridadi lakuibeba Ufaransa

Loic Remy 

Mabingwa watetezi wa taji la Ulaya waliongatuliwa kama wamiliki wa Kombe la Dunia, Uhispania, waliongezewa mawazo zaidi Alhamisi usiku pale bao spesheli lake straika mpya wa Chelsea, Loic Remy, lilipowanyamazisha 1-0.

Remy alifungulia mkwaju mzito uliopaa wavuni dakika ya 73 baada ya kuunganishiwa krosi na Mathieu Valbuena katika mechi ya kirafiki ambayo wenyeji walistahili kuibuka na ushindi dhidi ya mabingwa hao wa dunia waliongatuliwa kutoka utukufu wao nchini Brazil.

Huku wakikosa vigogo mashuhuri wastaafu, Xavi Hernandez, Xabi Alonso na David Villa, Uhispania waliendeleza mtindo waliozoea wa kumiliki mpira kwa kipindi kirefu na pasi fupi bila ya kutishia ngome ya wenyeji wao.


Ufaransa walionesha makali zaidi mbele ya lango kwa kubuni nafasi bora zaidi kufunga huku mshambuliaji maarufu, Karim Benzema, akitia wavuni baada ya nipe-nikupe ya kuvutia lakini goli hilo likakataliwa kwa makosa ya kuotea dakika nne baada ya kipindi cha lala salama kuanza.

Picha za runinga zilionyesha waamuzi walikosea kukataa bao hilo lakini bidii yao ilizawadiwa wakati Remy, aliyeingia kama mchezaji wa akiba, alipozamisha goli la kuamua mechi hiyo.
“Timu zote zilitoshana nguvu lakini walifanikiwa kubuni nafasi zao kwa haraka ingawa tulidhibiti mchezo,” kocha wa Uhispania, Vincente Del Bosque, alisema.