Tuesday, November 4, 2014

ETI YANGA INA MCHEZAJI MMOJA TU ANAYECHEZA KIKOSI CHA KWANZA

KOCHA wa Kagera Sugar, Jackson Mayanja amesema kuwa kiungo Mbrazil wa Yanga Andrey Coutinho ndiye mchezaji pekee anayeibeba Yanga kwa sasa lakini akadai hiyo kwa sasa inacheza kama imechoka tofauti na msimu uliopita.

Mayanja, raia wa Uganda alisema; “Yanga wana kiungo mmoja mzuri ambaye ni Coutinho, anajua kucheza kwa kasi na ana akili nzuri ya soka. Huyo ndiye mchezaji anayeweza kuisaidia Yanga kwani kwa staili wanayocheza Yanga kwasasa ni ile isiyoweza kuwapa ushindi kirahisi.”

“Yanga kwa msimu huu imepoteza kasi tofauti na msimu uliopita na ili warudishe kasi hiyo lazima benchi la ufundi lifanye kazi ya ziada,” alisema kocha huyo ambaye timu yake iliichapa Yanga bao 1-0 Jumamosi iliyopita japokuwa alikuwa jukwaani akitumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Katika hatua nyingine kocha huyo ametamka wazi kuwa Yanga haikuwa na sababu ya kumsajili Mbrazil Geilson Santos ‘Jaja’ na badala yake wangetulia na wachezaji wazawa wenye uwezo mkubwa.


“Jaja bado sana, kiwango chake hakiendani hata na wachezaji wengine wa Kitanzania, hapa Tanzania kuna wachezaji wengi ambao wana uwezo mkubwa kuliko Jaja ingawa inawezekana ni muhimu kwa kocha wake (Marcio Maximo) kutokana na mahitaji yake timu inapokuwa uwanjani.

“Yanga ina wachezaji kama Tegete (Jerry), Bahanuzi (Said) na Hamis Kiiza ambao wote ni wachezaji wa kiwango cha juu kuliko nilivyomtazama huyo Jaja kwenye mchezo dhidi yetu na hata michezo mingine Yanga imekuwa ikicheza msimu huu,” alisema Mayanja baada ya timu yake kuilaza Yanga bao 1-0.