Monday, November 3, 2014

Phiri:Sare Simba siri nzito

Wakati Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, akisema matokeo ya sare ambayo timu yake imeendelea kuyapata katika mechi za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara yana siri nzito na yanazidi kumchanganya, Mecky Maxime anayeinoa Mtibwa Sugar amekivulia kofia kikosi cha Mzambia huyo kwa kusema kinakosa bahati tu.

Simba juzi iliendelea kupata sare na kufikisha pointi sita katika mechi sita walizocheza katika Ligi ya Bara msimu huu ambayo ilianza kupigwa kwenye viwanja mbalimbali nchini tangu Septemba 20, mwaka huu.

Sare ya juzi ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar waliyoipata Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani hapa, imeifanya timu hiyo kuendelea kusuasua msimu huu huku ikiwa benchi la ufundi likiwa limepewa mechi mbili za kusaka matokeo mazuri.

Akizungumza na gazeti hili jana, Phiri, alisema matokeo ya sare ni ya kawaida katika soka lakini kwa upande wa Simba msimu huu yamekuwa yakizungukwa na 'siri' ndani yake, hivyo yanampa wakati mgumu. Phiri alisema anaumia kuona timu hiyo ikicheza vizuri lakini ikishindwa kupata pointi tatu tangu msimu wa ligi ulipoanza na kuwanyima furaha wachezaji, mashabiki na viongozi wa klabu hiyo.

Alisema wachezaji wanatengeneza nafasi lakini kuzitumia inakuwa tatizo na kumaliza dakika 90 wakiwa na maumivu.

"Matokeo ya sare ni sehemu ya mchezo, lakini inapokuwa katika mechi sita na kwa namna timu ilivyojiandaa inanichanganya, sielewi na hata wachezaji hawaelewi, hali hii inatuumiza sana," alisema Phiri.

Kocha huyo aliongeza kwamba anashindwa kuelewa ni namna gani Mtibwa Sugar walisawazisha bao lao ambalo walilipata katika kipindi cha kwanza na kufanya wagawane pointi. "Sina la kusema, kama tumepewa mechi mbili wao viongozi ndiyo wataamua, ila rasmi mimi hawajanieleza kuhusiana na tamko hilo," Phiri aliongeza.

Kocha huyo pamoja na kikosi chake kilirejea jijini Dar es Salaam juzi usiku baada ya mechi na leo jioni wanatarajia kuanza mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa Jumapili Novemba 9, mwaka huu dhidi ya Ruvu Shooting utakachezwa kwenye Uwanja wa Taifa.

MEXIME: SIMBA HAINA BAHATI
Licha ya kulazimisha sare katika mechi yake ya juzi, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mexime, amesema Simba ina kikosi kizuri na matokeo ya sare mfululizo wanazopata katika mechi za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara yanatokana na kukosa bahati.

Mexime alisema mechi yao ya juzi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 ilikuwa ngumu na Simba wanatakiwa kuwa na subira kwa sababu ligi ni ngumu na dakika 90 ndizo zinazotoa matokeo ya mechi.

Beki huyo na nahodha wa zamani wa timu ya Mtibwa Sugar na timu ya Taifa (Taifa Stars), alisema bado ligi ni 'mbichi' hivyo Simba inaweza kuamka na kupata matokeo mazuri tofauti na inavyoonekana sasa kwenye msimamo.

"Nani aliyesema ushindi lazima upatikane nyumbani, hii ni ligi, Simba ni wazuri na ninachoona mimi hawana bahati ya kushinda, si wabaya, mechi ilikuwa ngumu na kila upande ulipambana," alisema Mexime.

Mtibwa Sugar sasa imefikisha pointi 14 kati ya mechi sita ilizocheza na kuendelea kuongoza katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 14 ikifuatiwa na Coastal Union yenye pointi 11, mabingwa watetezi,  Azam na Yanga ambao kila mmoja ina pointi 10.