NAHODHA wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Mecky Mexime Kianga amesema kwamba safu mbovu ya ulinzi iliwaponza Simba SC kufungwa mahasimu wao, Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ilifungwa 2-0 na Yanga SC katika mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mabao ya Amissi Tambwe kipindi cha kwanza na Malimi Busungu kipindi cha pili.
Akizungumza kwa simu kutoka Turiani, Morogoro, Mexime amesema kwamba Simba SC wanatakiwa kufanyia kazi safu yao ya ulinzi, vinginevyo itaendelea kuwagharimu. "Kilichowaumiza Simba ni kutokuwa na safu imara ya ulinzi," amesema.
Kuelekea mchezo wake na Yanga SC, Mexime amesema kwamba Mtibwa Sugar ina ukuta imara hivyo haitapa shida kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu.
"Mabeki wangu wako vizuri zaidi ukilinganisha na waliocheza juzi kwa upande wa Simba, yaani (alitaja jina la beki) ndio wanamtegemea, kwangu bado hajanivutia," aliongeza beki huyo na nahodha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars.
Mtibwa Sugar wanatarajia kuikaribisha Yanga keshokutwa Jumatano katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.